Home News Yeriko Nyerere Akana Tuhuma za Uchochezi Facebook

Yeriko Nyerere Akana Tuhuma za Uchochezi Facebook

249
0
SHARE

MFANYABIASHARA, Yeriko Nyerere amekana mahakamani kutoa taarifa za upotoshaji kupitia mtandao wa Facebook, baada ya kusomewa maelezo ya awali katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.

Nyerere alisomewa maelezo yake jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri.

Wakili wa Serikali, Elia Athanas, alidai Oktoba 25, 2015 katika eneo lisilojulikana Dar es Salaam, Nyerere alichapisha taarifa za upotoshaji kupitia mtandao wa Facebook kuwa ‘piga kura leo huku ukikumbuka kifo cha Mwangosi, mateso ya Ulimboka na Kibanda, mateso ya kijana wetu wa JKT, ukikumbuka hayo fanya uamuzi sahihi bila ushabiki’.

Upande wa Jamhuri uliendelea kudai kuwa Oktoba 24, 2015 katika eneo lisilojulikana  Dar es Salaam, Nyerere alichapisha taarifa za upotoshaji kupitia mtandao wa Facebook kuwa Taifa la Tanzania kuanzia siku hiyo halihitaji amani, linahitaji haki tu.

Pia, Oktoba 24, 2015 mshtakiwa anadaiwa kuchapisha taarifa za uongo kupitia Facebook kuwa siku hiyo mpaka siku ya kuapishwa Lowassa Taifa halihitaji amani bali linahitaji haki tu, amani ilishatoweka siku nyingi, kilichosalia ni uvumilivu tu.

Pia alidaiwa kuchapisha taarifa za uongo kuwa njia sahihi ya kulitibu taifa hili ni kwa dola dharimu kutenda haki hata kama itawauma.

Ilidaiwa Nyerere aliandika kwenye mtandao huo kuwa “Uchaguzi huu ni vita, anayedhani ni demokrasia apimwe akili. Kwamba “hii ni vita kati ya umma na dola, ni vita kati ya wema na ubaya, ni vita kati ya shibe na njaa, ni vita kati ya maskini na matajiri, CCM sio chama cha siasa kwa sasa, ni muungano wa kihalifu unaolindwa na baadhi ya watumishi wa vyombo vya dola.”

Mshtakiwa huyo anadaiwa Agosti 24, mwaka 2015 alichapisha taarifa nyingine ya upotoshaji kupitia mtandao huo wa Facebook kwamba Kikwete yupo Ngurdoto Arusha na wakuu wote wa mikoa na wilaya Tanzania nzima pia wakuu wa vyombo vya dola na wanadhimu.

Kwamba wakuu wa mikoa wanaelezwa kwanza kuwa NEC kwa kushirikiana na CCM tayari wameshatengeneza kura bandia kwa kutumia mfumo wa kalamu za Kichina.

Pia, wanaamuliwa kuhakikisha wanahujumu kampeni za Ukawa kwa kutumia vyombo vya dola, wanaagizwa kuhakikisha kamatakamata ya vijana bodaboda wiki moja kabla ya uchaguzi na zaidi ni wakuu hao wa mikoa wanaagizwa  wakawaagize wakuu wa wilaya kote nchini kuhakikisha wanalinda maslahi ya CCM siku ya uchaguzi.”

Nyerere anadaiwa kuwa Septemba 3, 2015 katika eneo lisilojulikana alichapisha taarifa za upotoshaji kupitia mtandao wa Facebook  kuhusu uwapo wa akaunti ya benki ya kughushi inayomilikiwa na Mtanzania katika benki ya HSBC tawi la North London ikionyesha CCM imemwekea Dk. Slaa  pauni milioni 1.5 kupitia kwa mchumba wake Josephine Mshumbusi ikiwa ni rushwa ili kushinda uchaguzi 2015.

Mshtakiwa huyo andaiwa kuchapisha taarifa hizo za upotoshaji akiwa na lengo la kupotosha umma katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Hata hivyo, mshtakiwa alikiri kukamatwa kuhojiwa na polisi na kufikishwa mahakamani kwa mashtaka hayo pamoja na jina na anuani yake.

Mshtakiwa alikana maelezo yote kwamba hayatambui na kwamba hajatenda kosa hilo.

Hakimu Mashauri alisema kesi hiyo itaanza kusikilizwa ushahidi wa Jamhuri Julai 6, mwaka huu.