Home News Wabunge watapeliwa Viwanja Dodoma

Wabunge watapeliwa Viwanja Dodoma

175
0
SHARE
HUKU serikali ikitangaza msako mkali wa viwanja 34,000 visivyoonekana licha ya kupimwa katika Manispaa ya Mji wa Dodoma, imebainika baadhi ya wabunge wametapeliwa mamilioni ya shilingi na baadhi ya waendaji wa iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) wakiahidiwa kupatiwa viwanja.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alifichua utapeli huo alipozungumza na wanachama wa Chama cha Wapimaji na Ramani Tanzania (IST) jana.
Alisema kutokana na kufutwa kwa CDA na Rais John Magufuli, amekuwa akifutwa na watu waliotapeliwa viwanja na mamlaka hiyo wakiwamo baadhi ya watunga sheria.
Mei 15, mwaka huu, Rais Magufuli aliivunja mamlaka hiyo na kuhamishia shughuli zake kwa manispaa mara baada ya wakazi wa Mkoa wa Dodoma kulalamikia utendaji wa chombo hicho kilichoundwa kwa tamko la Rais la mwaka 1973.
“Walinifuata wakaniambia ‘sasa itakuwaje tuliwapa fedha Sh. milioni tano (kwa kila aliyehitaji kiwanja) kwa ajili ya viwanja lakini Rais akavunja mamlaka?” alisema.
Alisema uuzaji huo wa viwanja ulifanywa kinyume cha taratibu na baadhi ya wapimaji pamoja na maofisa ardhi wa mamlaka hiyo waliokuwa wakiwafuata watu na kuwaambia kuwa wanauza viwanja kwa bei hiyo.
“Mabwana ardhi wanauza kwa madalali, wamefungua maduka ya viwanja nje ya CDA, tunajua ujanja wenu mnaikosesha serikali mapato,” alisema.
Aliongeza kuwa wapimaji na maofisa ardhi hao walikuwa wakiuza viwanja vilivyopo eneo la Itega kwa Sh. milioni 25 wakati CDA ilikuwa ikiuza kwa Sh. milioni tano.
Alisema wamegundua kuwa kuna baadhi ya watumishi wa mamlaka hiyo walikuwa wanashikilia viwanja hadi 100 badala ya kuviuza kwa wananchi.
Alisema wapimaji hao na maofisa ardhi walikuwa wakimfuata mtu na kuchukua fedha kwa ajili ya kununua kiwanja na kisha kumletea mteja ankara ya CDA.
Lukuvi alisema serikali imebaini mamlaka hiyo ilipima viwanja 60,000, lakini vilivyopewa hati miliki ni 26,000 tu.
“Mnaikosesha serikali mapato maana hii, hakuna hati ambazo zimetolewa. Sasa nyie mliopo hapa (wapima ardhi waliokuwa CDA, mkawapelekee salamu kuwa tunawafahamu hao watumishi walioficha viwanja hivyo wavitoe haraka la sivyo vitawatokea puani,” alisema.
Alisema kuwa tayari ameshapata majina ya maofisa wote waliohusika kuficha viwanja hivyo huku akiahidi kuwa kufikia Desemba mwaka huu, vyote vitakuwa vimeshaonekana vilipo na wanaovimiliki.
Aliongeza kuwa katika maeneo mengi, wapimaji wa ardhi ambao watumishi wa serikali wameiibia nchi kwa kupeleka michoro ambayo haijakamilika.
“Wapimaji wa binafsi wanapeleka michoro iliyokamilika kwa sababu wanalipwa kutoka na idadi ya viwanja,” alisema.
Alisema kuna maeneo mengine viwanja vilishapimwa miaka 10 iliyopita lakini bado vinauzwa kutokana na wizi huo.
Waziri huyo alikigeukia chama hicho kwa kutochukua hatua kwa wanachama wanaonekana kukiuka maadili ya kazi.
“Kwanini hamuwafuti uanachama? Wanafanya wizi na uharibifu au ndiyo mlivyosomea? Nataka nikija mwakani hapa, mniambie kwamba mmewafuta wangapi, najua wapo hata wizarani wapo ama mnataka niwataje?” Alihoji.
Awali Rais wa IST, Martins Chodata, alimuomba waziri huyo kuingilia kati mgogoro kati ya wapimaji na wataalamu ambao alidai umekuwa ukirudisha nyuma ufanisi.