Home Latest News Mjue Vizuri Edward Ngoyai Lowassa.

Mjue Vizuri Edward Ngoyai Lowassa.

202
1
SHARE
Waziri mkuu, msitaafu Edward Lowassa. (Picha na maktaba simamiaMediaGroup)
kutoka simamia.com na (Shaaban)

Kwa Ufupi: Hii ni habari kuhusu maisha Halisi ya Waziri mkuu msitaafu Edward Lowassa Imeandaliwa kwa kuzingatia maadili na heshima ya tasnia ya Habari.

simamiateam@gmail.com / kisleufahari@gmail.com

Dar Es salaam. Edward Lowassa alizaliwa Agosti 26, 1953 katika Kijiji cha Ngarash, Monduli na ndiye mtoto mkubwa wa kiume kwa Mzee Ngoyai Lowassa (atafikisha miaka 64 Agosti mwaka huu). Alianza kusoma katika Shule ya Msingi Monduli kati ya mwaka 1961–1967.

Kisha akaendelea kwenye Shule ya Sekondari Arusha kwa kidato cha kwanza mpaka cha nne kati ya mwaka 1968 – 1971, kabla ya kumalizia kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Milambo mkoani Tabora mwaka 1972–1973.

Alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1974–1977 na kuhitimu Shahada ya Sanaa katika Elimu (B.A Education) na baadaye Chuo Kikuu cha Bath Uingereza kwa Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Maendeleo (mwaka 1983–1984).

Baada ya kumaliza chuo kikuu, Lowassa alifanya kazi ndani ya CCM akiwa ofisa wa ngazi ya juu kuanzia wilaya, mkoa na baadaye makao makuu kati ya mwaka 1977–1989.

Aliajiriwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Mikutano ya Kimataifa Arusha (AICC), mwaka 1989–1990.

Lowassa amemuoa Regina na wana watoto watano, wasichana wawili na wavulana watatu. Watoto hao ni Fredrick, Pamella, Adda, Robert na Richard.

MBIO ZA UBUNGE

Lowassa alichaguliwa kuwa Mbunge kupitia kundi la Vijana ndani ya CCM na akashikilia nafasi hiyo kati ya mwaka 1990 hadi 1995 na mwaka 1993 aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais (Haki na Mambo ya Bunge), kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Ardhi na Makazi akiwa Waziri mwaka 1993–1995.

Kwenye Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi (mwaka 1995), Lowassa alishinda ubunge kwa asilimia 87.3. Alikaa bila uteuzi wowote kwa miaka miwili. Mwaka 1997–2000, Rais Benjamin Mkapa alimteua kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na Kuondoa Umasikini).

Kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 aligombea tena ubunge wa Monduli na kushinda kwa mara ya tatu. Rais Mkapa akamteua kuwa Waziri wa Maji na Mfugo hadi mwaka 2005.

Kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2005, aligombea ubunge na kushinda kwa asilimia 95.6. Rais Jakaya Kikwete alimteua kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania na Bunge likamthibitisha kwa kura 312.

Uwaziri mkuu wa Lowassa ulikoma Februari 2008, alipojiuzulu kutokana na kashfa ya Richmond. Kamati Maalumu ya Bunge ya watu watano iliyoongozwa na Dk Harrison Mwakyembe ilisisitiza kuwa wizara ya Nishati na Madini na Ofisi ya Waziri Mkuu ndizo zinazopaswa kubeba lawama ya uingiaji wa mkataba mbovu na Richmond, kampuni ambayo uchunguzi ulionyesha kuwa ni ya mfukoni mwa watu huku Serikali ikilazimika kulipa mabilioni ya fedha katika mkataba ambao una upungufu makubwa.

Wakati Lowassa analitaarifu Bunge kuwa amemuandikia Rais barua ya kujiuzulu, alisisitiza kuwa “…anafanya hivyo ili kulinda taswira ya chama chake na Serikali na kuwa shida ya wabaya wake ni u-waziri mkuu na siyo kingine…”

Baada ya kujiuzulu, Lowassa aligombea ubunge kwa mara nyingine Monduli (mwaka 2010) na kupata asilimia 90.93 ya kura zote.

MBIO ZA URAIS

Lowassa ni miongoni mwa wana CCM 17 waliochukua fomu kuwania urais mwaka 1995 lakini aliyepitishwa ni Mkapa.

Mwaka 2005, hakugombea urais ila alikuwa na mipango ya muda mrefu ya kumsaidia rafiki yake, Kikwete na inadaiwa kuwa makubaliano ya Kikwete na Lowassa yalikuwa kwamba mwenzake akishaongoza nchi kwa miaka 10 (yaani 2005 – 2015) atamtengenezea njia 2015 – 2025.

Kabla mipango hiyo haijatimia ndipo Lowassa akapata kile ambacho Kikwete anakiita “ajali ya kisiasa”. Lakini hata baada ya ajali ya kisiasa kutokea, inasemekana walikuwa na makubaliano mengine kuwa “Kikwete angesaidia kumsafisha rafiki yake” ili mwaka 2015 ufikapo aweze kumuachia Ikulu ya Magogoni.

Kama kuna mtu nchi hii ametoa michango mingi ya rasilimali fedha katika kuchangia misikiti, makanisa, vijana, vikundi, harambee na vinginevyo, hakuna kama Lowassa. Hayo inasemekana aliyafanya kwa ajili ya kutengeneza mazingira ya kugombea urais.

Hatimaye mwaka 2015 akahamia CHADEMA ambaye huko ndipo alipofanikiwa kupata fursa ya kugombea urais.

UDHAIFU WAKE

Kuna msemo mmoja wa Kiingereza unaosema, “The bird with same feathers, flocks together” (Ndege wenye mabawa yanayofanana, huruka pamoja). Marafiki wakubwa wa Lowassa ni watu wenye pesa na matajiri.

Hata mwaka 1995 inasemekana, moja ya mambo yaliyomfanya Mwalimu Julius Nyerere asimuone Lowassa kama chaguo, ni suala la uhusiano wake na matajiri na watu wenye fedha na ilifikia wakati mwalimu akahoji, “…kijana huyu anatoa wapi fedha zote hizi?”

Alipokuwa Waziri Mkuu hakuonyesha makeke yake kwenye mapambano dhidi ya rushwa na hakutaka kujihusisha wala kujionyesha kuwa anawachukia wala rushwa. Pamoja na kuonyesha utendaji mzuri akiwa Waziri Mkuu, kipengele hiki kilimuangusha na hadi leo hii kokote kule anakokwenda hapendi kuzungumzia rushwa na wala rushwa.

Kwa mfano kashfa ya Richmond. Tangu kashfa hiyo ilipotokea, Lowassa hakuwahi kuiongelea tena na hajawahi kuwaeleza Watanzania alihusikaje na kama yeye hakuhusika ni kina nani waliohusika kwa majina. Ukweli ni jambo muhimu kwa mtu anayehitaji kuongoza nchi. Ukituhumiwa kwa kashfa kubwa kama ya Lowassa halafu unasema tu hukuhusika bila kueleza nani walihusika huku wewe ndiye ulikuwa Waziri Mkuu, inajenga taswira kuwa kuna jambo kubwa unalificha na husemi ukweli kwa jamii yako.

MPENDWA, UNAMZUNGUMZIAJE LOWASSA? Tuandikie hapo chini kwenye comment.

1 COMMENT

  1. Yote sawa kama Lowasa angetaka kutakasika kwa kasfa ya Lichimondi basi angewaelezea wanachi kua yeye akuudika na jammbo ilo nakama aliajizwa kutoka mamlaka za juu basi atwambie asitake yeye kufanywa kama chambo manake yeye ndoanaonekana kama mkosefu wajambo ilo,Mimi binafsi napenda Lowasa kuwa rais watanzania pia alijiandaa kwa mda mlefu,Ehee Mungu timiza malengo ya mtu uyu yaweza kuwa mkomboxi wawatanzania

Comments are closed.