Home Latest News Bilioni 700 tulizozipata Magufuli Anasitaili pongezi.

Bilioni 700 tulizozipata Magufuli Anasitaili pongezi.

314
0
SHARE
Wakati wakisaini mkataba wa makinikia.
kutoka simamia na (Shaaban)

Tangu kuwepo kwa zuio la usafirishaji wa mchanga wa dhahabu (makinikia) kwenda nje lililofanywa na Rais Dk. John Pombe Magufuli, nilieleza waziwazi kuwa ninamuunga mkono rais wangu na kwamba nitakuwa nyuma yake hatua kwa hatua juu ya kupigania rasilimali za Watanzania.
Hatimaye mazungumzo kati ya magwiji wa sheria na mambo ya mikataba ya madini na timu ya wataalam wa kampuni ya uchimbaji wa madini nchini, Barricks ambayo yamechukua muda mrefu kutokana na unyeti wake, sasa yamezaa matunda. Taarifa iliyotolewa leo inaonesha tunaanza tunaanza mwanzo mpya wa kuzilinda rasilimali zetu kwa vizazi vijavyo.
Kwangu na Watanzania wenzangu ni furaha isiyoelezeka, kuona tulichokipigania kinapatikana! Bado ninamuunga mkono rais wangu na ninatamka waziwazi: ‘Hongera Rais Magufuli kwa hatua nzuri uliyotufanya Watanzania tuifikie’!
Kwa nini ninampongeza Rais Magufuli? Ni kwa sababu kuna mambo mazuri mno kwa Watanzania ambayo yamefikiwa kwenye makubaliano kati ya pande hizo mbili. Makubaliano hayo ya kutia faraja ni pamoja na mosi; masharti yote yaliyopo katika sheria mpya ya madini iliyotungwa na bunge letu na kuhakikisha masharti hayo yanaingia kwenye mfumo wa fedha.
Pili; pande hizo mbili kukubaliana kuwa serikali itapata hisa katika migodi hiyo kwa asilimia 16 kama sheria ilivyotamka, lakini pamoja na kumiliki migodi hiyo kwa asilimia 16, kwenye mgao itakuwa ni asilimia 50 kwa 50.
Tatu; wamekubaliana kuwa migodi hiyo itaweka fedha zinazotokana na madini katika akaunti zilizopo hapa nchini tofauti na awali ambapo fedha hizo zilikuwa zikipelekwa nje ya nchi.
Nne; pia wamekubaliana kuwa, sasa ofisi za kampuni hiyo za London nchini Uingereza na Johannesburg, Afrika Kusini, katika siku za usoni zitahamishiwa Tanzania na makao makuu ya kampuni hiyo yawe jijini Mwanza ingawa wanaweza kuwa na ofisi nyingine sehemu nyingine.
Tano; wamekubaliana kuanzisha kampuni nyingine ya kusimamia na kuendesha migodi na makao makuu yake yatakuwa Mwanza na itaongozwa na mtendaji mkuu, mkurugenzi wa fedha na mkurugenzi wa manunuzi kutoka Tanzania huku serikali ikipata asilimia 16 na mgao wa asilimia 50 kwa 50 na kwamba serikali iwe na wawakilishi katika bodi ya wakurugenzi wa kampuni hiyo katika kila mgodi.
Sita; wamefikia makubaliano kuwa sehemu kubwa ya kazi zitolewazo mgodini, sasa kwa kiasi kikubwa inavyowezekana zitafanywa na kampuni za Kitanzania na Watanzania.
Saba; wamekubaliana kuimarisha huduma za kijamii katika maeneo yaliyo karibu na migodi.
Nane; wamekubaliana kuwa kila kampuni inayoendesha mgodi kuhakikisha inaachana na utaratibu wa kutumia wafanyakazi wa mikataba na badala yake kuajiri wafanyakazi wa kudumu ambao ni wazawa na hawatakaa katika makambi kama ilivyokuwa awali, badala yake kwenye makazi na familia zao na watajenga barabara ili wafanyakazi waweze kutoka kazini na kwenda makwao.
Tisa; pia Watanzania katika nafasi muhimu na za utaalam, wawafundishe wazawa ili baadaye waweze kujaza nafasi za uongozi.
Kumi; wamekubaliana kutenga bajeti maalum kwa ajili ya kuchangia utafiti wa kuendesha utafiti wa kuanzisha kiwanda cha kuchakata makinikia na kujenga maabara kubwa ya kupima makinikia.
Kumi na moja; wamekubaliana kuwa serikali itakuwa na umiliki wa madini yote (rare metals) kama zitapatikana na wao watabaki na dhahabu, shaba na fedha. Mafanikio ambayo si haba!
Kumi na mbili; wamekubaliana kuwa kesi na mashauri yote yatafanyika hapa Tanzania na siyo nje kama ilivyokuwa awali.
Lingine lililofikiwa makubaliano ambalo nalo ni kubwa ni suala la fidia ambalo awali lilionekana kuwa gumu sana na ndilo lililochukua muda mrefu, lakini mwisho wa siku tumelamba dume kwa kupata dola milioni 300 (zaidi ya Sh. bilioni 700).
Katika makubaliano hayo na mengine yote, Watanzania tuna kila sababu ya kumshukuru Rais Magufuli kwa azma ya kusimamia mambo haya kidete na kwa nguvu zote na kututia moyo na kuwaamini wataalam wetu badala ya kuleta wataalam kutoka nje.
Watanzania, tukubaliane kuwa asilimia 50 kwa 50 waliyokubaliana ni hatua kubwa mno na mazungumzo yaliyosalia tunaamini tutafikia muafaka.
Tutoe wito kwa baadhi ya Watanzania, waache kubeza mambo kama walivyofanya wakati rais alipogundua wizi huu mkubwa wa madini uliokuwa unafanyiwa taifa letu, leo sote tunaona manufaa ya kiongozi wetu wa nchi.
Nirudie tena kumpa heko Rais Magufuli na kumhakikishia kuwa Watanzania wapo nyuma yake katika kutetea rasilimali zetu!

-Eric Shigongo-

Nini maoni yako tuandikie hapo chini kwenye comment.