Home Politics Zitto: Matunda ya uongozi wa JK kunufaisha Wananchi

Zitto: Matunda ya uongozi wa JK kunufaisha Wananchi

361
0
SHARE
Kiongozi wa ACT - Wazalendo, Zitto Kabwe
Kiongozi wa ACT - Wazalendo, Zitto Kabwe
Kiongozi wa ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe

MGOMBEA ubunge wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amepongeza mafanikio yote ya Rais Jakaya Kikwete, yaliyopatikana katika mkoa wa Kigoma katika kipindi cha miaka kumi ya uongozi wake.

Zitto alitaja mafanikio hayo kuwa ni pamoja na miundombinu, ikiwemo ujenzi wa barabara za kiwango cha lami na ujenzi wa Daraja la Kikwete katika Mto Malagarasi, ambalo lilizinduliwa juzi na Rais Kikwete.

“Juzi Rais Kikwete mwenyewe kasema ni namna gani tulipambana pamoja kwa ajili ya ujenzi wa daraja la Malagarasi, alisema kwamba ilibidi amchukue Zitto kwenda kuwashawishi wazungu watoe fedha za ujenzi wa daraja hilo.

Napongeza, sio tu kwa daraja hilo, lakini pia na miradi mingine ambayo imefanyika katika mkoa huu ikiwa ni pamoja na barabara,” alisema Zitto. Akizungumza na maelfu ya wakazi katika mkutano wa kampeni Kigoma Mjini, Zitto aliwaomba wananchi kuichagua ACT Wazalendo ili waweze kupata mabadiliko ya kweli ya maendeleo.

“Ninachowaomba mnitafutie kura, tupate kura nyingi tushinde mkoa mzima, kipeperushi kina mambo yetu yote ambayo tunaahidi kuyafanya na tusipoyafanya mtudai kwa hayo na mtuwajibishe,” alisema Zitto, ambapo pia alinadi ilani ya chama chake na kuwanadi wagombea wa udiwani katika jimbo hilo.

Zitto alisema anaomba ridhaa, atumwe kwa miaka mitano aende bungeni kupigania maendeleo ya mkoa wa Kigoma ili ubadilike na kupanda hadhi kuwa jiji la Kigoma. “Mambo hayo yaliyoko kwenye kipeperushi ambayo ndiyo vipaumbele chetu, chini nimeweka sahihi yangu, kila mwaka ukipita unainua unaangalia nini kimefanyika unatia tiki, miaka mitano ikitimia aangalieni yapi hayana tiki, mje kunisuta na kama sina maelezo basi mniwajibishe,” alisema Zitto.

Zitto alisema ameamua kugombea ubunge kwa jimbo la Kigoma Mjini ili kuufanya mkoa huo, uwe wa kibiashara na viwanda, kulingana na fursa mbalimbali zilizopo na rasilimali zake, ambazo ni pamoja na samaki na kilimo cha migazi. Aliahidi kutetea wananchi hao kwa kuwawezesha ili wajisimamie wenyewe katika shughuli zao.

Alisema kwamba wakimchagua, watakuwa wamepata mbunge mjanja, anayetazama mbali na ambaye ataweza kupanua miradi yao kuleta maendeleo. Pia, Zitto aliahidi kushirikiana na wabunge wenzake, kuanzisha benki ya Kigoma ili watu ambao watahitaji mikopo, waweze kukopa kuendeleza biashara zao.